logo

Watu 18 wauawa kufuatia vita kati ya waasi na majeshi ya Sudan Kusini

Watu kumi na wanane wameuawa kufuatia mapigano kati ya vikosi vya usalama vya Sudan Kusini na waasi watiifu kwa makamu wa rais wa zamani Riek Machar. Maafisa wa serikali wamesema hayo leo na kuongeza mapigano yalitokea Jumamosi usiku katika eneo la Upper Nile. Msemaji wa jeshi Santo Domic Chol ameliambia shirika la habari la ujerumani DPA kwamba wanajeshi wanane wameuawa pamoja na waasi 10, kufuatia shambulio ambalo lilifanywa katika kambi ya jeshi ililoko jimbo la Latjor. Msemaji wa waasi Paul Gabriel Lam, ameliambia DPA kuwa wapiganaji wake walikuwa wakijibu mashambulizi ya serikali katika maeneo yao. Wiki iliyopita, rais wa Sudan Kusini Salva Kiir alitangaza hali ya hatari katika jimbo jingine la Lakes baada ya mapigano ya kikabila kuzuka na kusababisha vifo vya takriban watu 100.

Leave a reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *