logo

Watu 33 wapoteza maisha katika ajali ya treni ya mizigo DRC

Watu 33 wamepoteza maisha siku ya Jumapili asubuhi, tarehe 12 Novemba, katika mkoa wa Lualaba wa kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya kutokea ajali ya treni ya mizigo ambayo imepelekea kujeruhiwa pia watu wengine kadhaa miongoni mwa abiria haramu karibu na mji wa Buyofwe.

Treni hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Lubumbashi kuelekea Luena, katika mkoa  Lualaba. Mkuu wa mkoa wa Lualaba, Richard Muyej, amesema: “Hii ni ajali mbaya kabisa kuwahi kutoka katika mkoa huu.”

“Ajali hiyo ilitokea mapema Jumapili asubuhi katika kijiji kimoja kilichoko umbali wa kilomita 25 kutoka mji wa Lubudi, kuelekea Luena. Treni hiyo iliacha njia na kutokana na kuwa ilikuwa imebeba matangi ya mafuta ya gari, ilisababisha kuwaka moto mkubwa,” alisema Muyej .

Taarifa zinasema kuwa, treni hiyo ilikuwa ikisafirisha matangi 13 ya mafuta wakati ilipotoka kwenye njia ya reli na kuanguka bondeni wakati ilipokuwa inapanda mlima na kupelekea matangi hayo ya mafuta kuteketea kwa moto.

Maafisa wa Shirika la Kitaifa la Reli DRC, SNNC, wamesema wanachunguza chanzo cha ajali hiyo ambacho bado hakijajulikana.

Ajali za treni hutokea mara kwa mara Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na kuzeeka reli, vichwa vya treni na mabehewa na pia uzembe katika utekelezaji wa sheria za usalama wa safari za treni.

Leave a reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *