logo

Upinzani Kongo DR wapinga tarehe ya uchaguzi iliyotangazwa na CENI

Vyama vya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimepinga tarehe ya uchaguzi iliyopendekezwa na Tume ya Uchaguzi CENI hivi karibuni.

Augustin Kabuya, msemaji wa chama kikuu cha upinzani nchini humo UPDS amesema, “hatukubaliana na ratiba ya uchaguzi iliyotolewa na CENI, tunachotaka kuona kikifanyika ni Rais Joseph Kabila aachie ngazi kabla ya Disemba 31 mwaka huu.” Mwisho wa kunukuu.

Kinara wa upinzani nchini humo Moise Katumbi ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa “Hatukubaliana na tarehe hiyo ya serikali ambayo ipo mamlakani kinyume cha sheria. Wanataka tu kuona hakuna uthabiti Kongo huku wakiwahangaisha wananchi. Kabila lazima aondoke.” Mwisho wa kunukuu.

CENI siku ya Jumapili ilisema kuwa uchaguzi wa rais wa kumtafuta mrithi wa Rais Joseph Kabila utafanyika Disemba 23, mwaka ujao wa 2018.

Mkuu wa tume hiyo, Corneille Nangaa amewaambia waandishi habari mjini Kinshasa kuwa watu 43 milioni wamesajiliwa kama wapiga kura nchini humo hadi sasa, na kwamba matokeo ya uchaguzi huo yatatangazwa Januari 9 , 2019 na rais kuapishwa Januari 13.

Uchaguzi huo ulikuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2016 na umeahirishwa mara kadhaa hadiĀ  sasa.

Leave a reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *